KESHA LA ASUBUHI JULAI 16/017/2025
Kondoo wa Kweli Wanamsikia Mchungaji wa Kweli Julai 16
"Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja." —Yohana 10:16
Kweli unapaswa kuwasilishwa kwa hekima, upole na wema wa Mungu. Unapaswa kutoka kwenye moyo ambao umelainishwa na kufanywa kuwa mwenye huruma... Hebu maneno yetu yawe ya upole tunapotafuta kuongoa roho. Mungu atakuwa hekima kwake yeye atafutaye hekima kutoka kwenye chanzo cha mbinguni.
Tunapaswa kutafuta fursa kila upande, tukikesha na kuomba, na kuwa tayari wakati wote ili kutoa sababu ya tumaini lililo ndani yetu, kwa upole na kicho. Tusije tukaivutia isivyofaa nafsi moja ambayo Yesu alifia; tunapaswa kudumisha mioyo yetu katika uadilifu kwa Mungu, ili fursa inapojitokeza, tupate maneno sahihi ya kusema kwa wakati unaofaa.
Kama utaichukua hivyo kazi ya Mungu, Roho wa Mungu atakuwa msaidizi wako. Roho Mtakatifu atayafanyia kazi maneno yaliyosemwa kwa upendo kwa ajili ya roho. Ukweli utakuwa na nguvu ihuishayo unaposemwa chini ya mvuto wa neema ya Yesu.
Mpango wa Mungu unapaswa kugusa moyo kwanza. Semma ukweli, na umruhusu Yeye kuendeleza nguvu na kanuni ya ubadilishaji. Usifanye rejea kwa yale wasemayo wapinzani, bali uruhusu ukweli pekee uendelezwe. Ukweli unaweza kukata haraka. Lifunue Neno waziwazi katika ushawishi wake wote.
Wakati maonjo yanapozidi karibu nasi, ndivyo utengano na umoja vitakavyoonekana kati yetu. Baadhi ya wale ambao sasa wako tayari kuchukua silaha za vita, katika wakati wa hatari halisi, watadhihirisha kuwa hawajajenga juu ya mwamba imara; watakubali majaribu.
Wale waliopata nuru kuu na fursa za thamani lakini hawakuziboresha, watatoka kwetu kwa kisingizio kimoja au kingine. Wakiwa hawajapokea upendo wa ukweli, watachukuliwa na udanganyifu wa adui; watazisikiliza roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani, na kujitenga na imani.
Lakini kwa upande mwingine, wakati dhoruba ya mateso itakapotokea juu yetu, kondoo wa kweli wataisikiliza sauti ya Mchungaji wa kweli. Juhudi za kujikana nafsi zitatolewa ili kuokoa waliopotea, na wengi waliotanga mbali na zizi watarejea ili kumfuata Mchungaji Mkuu.
Watu wa Mungu watakusanyika pamoja na kumkabili adui kwa mshikamano. Kwa kuzingatia hatari ya kawaida, ugomvi wa kutaka ukuu utakoma; hakutakuwa na mabishano juu ya nani atahesabiwa kuwa mkuu zaidi. Hakuna hata mmoja wa waumini wa kweli atakayesema: “Mimi ni wa Paulo; Mimi wa Apolo; Mimi ni wa Kefa.” Ushuhuda wa wote utakuwa: “Ninashikamana na Kristo; Ninafurahi ndani Yake kama Mwokozi wangu binafsi.”
Upendo kwa Yesu na kwa ndugu zetu utathibitisha kwa ulimwengu kwamba tumekuwa pamoja na Yesu na kujifunza Kwake. Kisha ujumbe wa malaika wa tatu utakua kufikia kilio kikuu, na dunia yote itaangaziwa na utukufu wa Bwana.
(Testimonies for the Church 6:400–401)
Comments
Post a Comment