KESHA LA ASUBUHI 15/07/2025 Kumpata Kondoo Aliyepotea
KESHA LA ASUBUHI JULAI 15- 2025
Kumpata Kondoo Aliyepotea
"Naye akimwona, amini nawaambia, humfurahia huyo zaidi kuliko wale tisini na tisa wasiopotea." —Mathayo 18:13
Yesu angependa kuhimiza thamani ya nafsi ya mwanadamu juu ya mioyo na akili za wanafunzi Wake. Anadai ushirikiano kwa shauku ya wafuasi Wake katika kuwaokoa wenye dhambi waliopotea. Kuna kondoo mmoja alipotea, idadi ndogo sana katika hesabu; na bado Yesu anamwakilisha mchungaji kuwa aachaye wale tisini na tisa, na kwenda milimani kutafuta yule mmoja aliyepotea.
Sasa ni kwa nini basi wana na binti za Mungu wamebweteka, hawajali roho ambazo zinapotea karibu yao? Ni kwa nini washiriki wa kanisa wako tayari sana kuacha mzigo wote kuwa juu ya mabega ya mchungaji? Ni kosa kubwa jinsi gani, ikiwa kila raia wa neema anapaswa kuwa na sehemu ya kufanya katika kuokoa wale waliopotea.
Yesu amempatia kila mtu kazi yake, na juhudi binafsi lazima ziwekwe ili kuokoa wanaopotea. Mtendakazi lazima awe na maombi mengi ya sirini; kwa maana kazi hii inahitaji hekima kubwa sana katika sayansi ya kuokoa roho. Yesu alisema, “Mimi ndimi nuru ya ulimwengu; yeye anifuata hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.” Aliwaambia pia wanafunzi Wake, “Ninyi ni nuru ya ulimwengu.”
Amelifanya kanisa kuwa bohari ya ukweli mtakatifu. Aliliachia kanisa Lake uwakili wa ukweli mtakatifu, na ni kazi ya kanisa kuendeleza utume wa kuuokoa ulimwengu. Yeye ni Jua la haki, ambaye anatoa miale angavu kwa wafuasi Wake; na wao, kwa upande wao, wanapaswa kuangaza nuru Yake kwa wengine. Wanalazimika kuwa wawakilishi Wake kwa ulimwengu. Wakiinamini Yesu kuwa Mwokozi wao binafsi, wanaichukua kazi pale Alipoiachia.
“Pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote,” alisema Yesu; bali tukiwa pamoja Naye tunayaweza mambo yote. Kuna idadi kubwa, kubwa sana ya kondoo wanaotangatanga na waliopotea ambao wameangamia katika majangwa ya pori la dhambi, kwa sababu tu hakuna mtu aliyewafuata, kuwatafuta na kuwarudisha zizini. Yesu anatumia mfano wa kondoo aliyepotea ili kuonesha hitaji la kuwatafuta wale waliotanga mbali Naye; kwa maana kondoo anapopotea hawezi kurejea zizini pasipo msaada. Lazima atafutwe, lazima achukuliwe ili kurejeshwa zizini.
Mbingu yote inapendezwa na kazi ya kuwaokoa waliopotea. Malaika wanaangalia kwa shauku kuu ili kuona ni nani atakayewaacha wale tisini na tisa, na kisha kwenda kwenye tufani na dhoruba na mvua hata porini jangwani ili kutafuta kondoo aliyepotea.
Waliopotea wako wengi karibu nasi, wakiangamia na kwa huzuni wakipuuzwa. Lakini ni wenye thamani kwa Mungu, walionunuliwa kwa damu ya Yesu... Tunalazimika kutafuta na kuokoa wale waliopotea. Tunapaswa kumtafuta kondoo mmoja aliyepotea, na kumrejesha zizini; na hili linawakilisha juhudi binafsi.
(The Review and Herald, Juni 30, 1896)
BWANA AKUBARIKI ENDELEA KUFUATILIA KWELI ZA THAMANI
Comments
Post a Comment