KESHA LA ASUBUHI JULAI 19 /07/ 2025 'KURUDISHWA ZIZINI NA MCHUNGAJI'

Kurudishwa Zizini na Mchungaji

“Kama vile mchungaji atafutavyo kondoo wake, siku atakapokuwa kati ya kondoo wake waliotawanyika, ndivyo nitakavyowatafuta kondoo wangu; nami nitawaokoa katika mahali pote walipotawanyika, katika siku ya mawingu na giza.” — Ezekieli 34:12

Kondoo aliyetanga mbali na zizi ni kiumbe mnyonge anayehitaji msaada kuliko wote. Ni lazima atafutwe na mchungaji, kwa kuwa hawezi kujua mwenyewe njia ya kurudi zizini. Ndivyo ilivyo kwa mtu ambaye ametanga mbali na Mungu: hajiwezi kabisa kama kondoo aliyepotea, na ikiwa upendo wa Mungu haukuja kumwokoa, asingeweza kupata njia ya kurudi kwa Mungu.

Mchungaji anayegundua kuwa mmoja wa kondoo wake amepotea hawezi kuzembea kwa sababu ya kundi ambalo limehifadhiwa kwa usalama na kusema, “Ninao wengi na wazima, na itanigharimu sana kwenda kumtafuta mmoja aliyepotea. Ngoja tu atakuja, kisha nitamfungulia mlango wa zizi na kumruhusu aingie.” La! Punde tu kondoo anapopotea, mchungaji anajawa na huzuni na wasiwasi. Anawahesabu tena na tena. Anapokuwa na uhakika kwamba kondoo mmoja amepotea, hawezi kulala. Anawaacha wale walioko salama zizini na kwenda kumtafuta yule aliyepotea.

Kadiri usiku unavyozidi kuwa wa giza na wenye dhoruba, na njia inavyozidi kuwa hatarishi, ndivyo shauku ya mchungaji inavyozidi kuwa kubwa na bidii yake ya utafutaji inavyozidi kuongezeka. Anafanya kila juhudi kumpata yule kondoo mmoja aliyepotea.

Ni faraja kiasi gani anaposikia kwa mbali kilio chake cha taabu kwa mara ya kwanza! Akifuatilia sauti ile, anapanda miinuko mikali zaidi, anakwenda katika kingo za majabali, akihatarisha maisha yake mwenyewe. Hivyo anatafuta, na kilio kile kinapozidi kufifia, kinamwambia kuwa yule kondoo yuko karibu kufa. Hatimaye juhudi zake huzaa matunda—aliyepotea anapatikana.

Mchungaji hamkaripii kwa sababu ya shida aliyomsababishia. Hamlaumu kwa kosa lake. Wala hajitahidi kumwongoza kwa mbali kuelekea nyumbani. Katika furaha yake, anamchukua kiumbe yule anayetetemeka mabegani mwake; kama amechubuka na kujeruhiwa, anamkumbatia katika mikono yake, akimsogeza karibu na kifua chake, ili joto la moyo wake mwenyewe lipate kumpa uhai. Kwa shukurani kwamba kutafuta kwake hakukuwa bure, anambeba na kumrudisha zizini.

Mungu ashukuriwe, hajawasilisha katika fikira zetu picha ya mchungaji mwenye huzuni akirudi nyumbani bila kondoo. Mfano huu hauzungumzii kushindwa, bali kuhusu matumaini na furaha ya urejeshwaji. Hapa kuna uthibitisho wa Mungu kwamba hakuna hata mmoja wa kondoo wa zizi la Mungu anayepotea anayeachwa bila msaada. Kila mmoja ambaye atajitoa kwa ajili ya kukombolewa, Kristo atamwokoa kutoka katika shimo la uharibifu na kutoka katika miiba ya dhambi.
(Lulu za Uzima, uk. 125–126)


Mungu akubariki karibu uendelee kufuatilia masomo haya na mengine mengi zaidi kupitia http://kwelizathamani.blogsport.com/

Comments

Popular posts from this blog

KESHA LA ASUBUHI JULAI 16/017/2025

KESHA LA ASUBUHI JULAI 18/07/2025 Tu Wachungaji Wasaidizi

KESHA LA ASUBUHI 15/07/2025 Kumpata Kondoo Aliyepotea